FIFA yapiga chini ombi la Zanzibar kuwa mwanachama kamili.

Shirikisho la Soka Duniani FIFA, limekataa ombi la Zanzibar kuwa mwanachama kamili kwa mantiki kuwa haiwezekani kwa nchi moja kuwa na mashirikisho mawili. 

Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Ahmad Ahmad amethibitisha taarifa hiyo na kusema  kuwa Zanzibar ilipewa uanachama bila kuzingatia baadhi ya vipengele muhimu ambavyo vipo wazi. 

-CAF haiwezi kuwa na Shirikisho mbili tofauti kutoka nchi moja, utambulisho wa nchi unatolewa na Umoja wa Mataifa ya Afrika AU", amesema Ahmad. 

Issa Hayatou 

Zanzibar ilipewa uanachama wa muda wa CAF mwezi Machi baada ya aliyekuwa Rais wa CAF Issa Hayatou kukubali ombi hilo wakati wakiendelea kusubiri maamuzi ya FIFA. 

Zanzibar ambayo ipo ndani ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania imekuwa ikisaka kwa muda mrefu kuwa mwanachama kamili wa  FIFA na CAF Lakini Mara kadhaa maombi yao yamekuwa yakipigwa chini.