Taifa Stars waicharaza tena Botswana, Msuva aibuka shujaa.

Timu ya Soka ya Tanzania 'Taifa Stars' imefanikiwa kuibuka na ushindi dhidi ya Timu ya Taifa ya Soka ya Botswana wa mabao 2-0.

Huo unakuwa wa kwanza kwa Taifa Stars, kucheza katika uwanja wa Uhuru baada ya miaka 11 walipowachapa DR Congo kwa mabao 2-0.

Dakika 45.

Taifa Stars waliuanza mchezo huo kwa haraka na kufanikiwa kuandika bao la kwanza kupitia kwa winga wa Difaa al Jadida Simon Msuva baada ya kupokea pasi murua kutoka kwa Mzamiru Yassin.

Baada ya bao hilo Botswana walicharuka na kuanza kuumiliki kwa kiasi kikubwa, huku dimba likitawaliwa na wao kwa umaridadi mkubwa.

Hata hivyo mchezo haukuonekana kuwa mzuri sana, kwa papatupapatu zikitawala zaidi kuliko ufundi Kwa wachezaji wote.

Hadi kipindi cha kwanza kinafikia tamati Stars walikuwa mbele kwa bao moja huku Botswana wao wakitoka wakiwa na ushindi wa umiliki wa mpira kwa asilimia 52 kwa 48.

Kipindi cha pili

Kipindi cha pili kilianza kwa Botswana kutafuta bao la kusawazisha kwa nguvu lakini juhudi zao zilizimwa katika dakika ya 61 baada ya Simon Msuva kuandika bao la pili.  

Baada ya bao hilo Kocha Salumu Mayanga alifanya mabadilko kwa kumtoa Shizya Ramadhan Kichuya na kumuingiza Farida Musa, lakini awali Mayanga alifanya mabadilko kwa kumtoa Mzamiru Yassin na kumuingiza Raphael Roth Daudi.

Dakika ya 72 Kiungo Farid Muda almanusura aipatie Stars bao la tatu, kwani mpira aliogongeana Simon Msuva kushindwa kujaa mguuni na kupiga shuti dhaifu lililotoka sentimita chache langoni mwa Botswana.

Kiungo wa Sony Sugar Hamisi Abdallah alidumu kwa dakika 81 akicheza soka safi hadi pale kocha Mayanga alipomtoa na kumuingiza kiungo mnyumbulifu Said Ndemla.

Hata hivyo dakika ya 83 Mbwana Samatta na Simon Msuva walitolewa na kuingizwa Emmanuel Martin na Elius Maguri.

Hata hivyo mabadiliko hayo hayakubadilisha chochote katika mchezo huo, kwani hadi Mwisho Taifa Stars 2-0 Botswana.

Rekodi muhimu

Ushindi umeweka rekodi kadhaa ikiwemo rekodi ya kuifunga Botswana mara mbili mfulululizo kwa idadi sawa ya mabao kwani Machi mwaka stars waliwafunga Botswana kwa mabao 2-0 mabao ya Mbwana Samatta.

Rekodi nyingine ni ya kipekee kwa Kocha Salumu Mayanga ambaye katika michezo 12 aliyoiongoza Stars amefungwa mchezo mmoja pekee, kichapo alichokipata katika michuano ya COSAFA dhidi ya Zambia.