Taifa International Friendly: Stars kuwasili nchini usiku wa kuamkia Jumanne.

Kikosi cha timu ya soka ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kinatarajiwa kuwasili usiku wa kuamkia Jumanne wakitokea nchini Benin walipotoka sare ya bao 1-1 na timu ya Taifa hilo.

Taifa Stars inarejea na wachezaji wote wanaocheza ligi ya ndani huku wale ambao wanacheza Soka la kimataifa akiwemo Abdi Banda na Simon Msuva wakitarajiwa kujiunga na timu zao wakitokea Benin.

Afisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini 'TFF' Alfred Lucas Mapunda, amesema kikosi hicho kitawasili usiku wa Saa 9 na nusu na mara baada ya kuwasili nchini kambi ya timu hiyo itavunjwa.

 -Timu yetu inatarajiwa kuwasili nchini usiku wa kuamkia Jumanne kwa ratiba ya ndege ni kwamba  itaingia majira ya saa tisa na nusu usiku au saa kumi kasoro, na ikishawasili kambi itavunjwa ili kupisha ratiba za ligi kuendelea,” amesema Alfred.

Sare ya Bao 1-1.

Taifa Stars walitoka sare ya bao 1-1 na Benin kwenye mchezo wa kirafiki uliopigwa Jumapili ya Novemba 12 katika uwanja wa Stade de l'Amitié uliopo katika Mji wa Cotonou, Benin.

Bao la Taifa Stars katika mchezo huo limefungwa na mshambuliaji wa kimataifa Elius Maguri katika dakika ya 51 licha ya Benin kutangulia katika dakika ya 30 kwa mkwaju wa penati.