Tanzia: Hamad Ndikumana Katauti afariki dunia.

Mshambualiaji wa zamani wa timu ya Stand United Hamad Ndikumana Kataut amefariki dunia usiku wa kuamkia leo akiwa nyumbani kwao nchini Rwanda.

Ndikumana aliwahi kuchezea klabu kadhaa barani Ulaya katika nchi za Ubelgiji, Israel, Cyprus na Ugiriki, na kusajiliwa na Stand mwanzoni mwa msimu wa 2015/16, lakini alishindwa kuisaidia timu hiyo kutokana na kushindwa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Taarifa kutoka kwa nahodha wa Timu ya Taifa ya Rwanda, Haruna Niyonzima amesema Ndikumana alikuwa na afya nzuri na wala hakuwa na shida yoyote wakati akifanya mazoezi na timu yake ya Rayon Sport kama kocha msaidizi hapo jana.

Sababu ya Kifo. 

Amesema mara baada ya mazoezi hayo alirudi nyumbani na kuanza kulalamika kuwa kichwa kinamuuma hadi pale mauti yalipomkuta usiku wa kuamkia Leo. 

-Alikuwa haumwi, lakini kapata tatizo jana baada ya mazoezi, alikuwa analalamika kichwa kinamuuma akarudi nyumbani kupumzika, wakati wakitafuta daktari hawakufanikiwa ikabidi wampeleke hospitali walipofika huko ndipo akafariki, inasemakana alikuwa na tatizo la Moyo," Niyonzima amesema kwa masikitiko.

Niyonzima amesema ni jambo ambalo limemuhunisha sana ukizingatia alikuwa ndiye mchezaji ambaye alimpokea na kumfundisha mengi akiwa katika timu ya taifa ya Rwanda.

Ndikumana ambaye amewahi kutamba na vilabu kadhaa anatajwa kufariki akiwa na umri wa miaka 39, pia anakumbukwa kwa kumuoa mrembo kutoka kiwanda cha filamu za Kibongo Irene Uwoya na kufanikiwa kupata mtoto mmoja wa kiume anayeitwa Krish.