VPL: Raundi ya 13 inogile, Simba kubaki kileleni?

Ligi kuu soka Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea tena Jumamosi, Januari 13 mwaka huu baada ya kusimama kwa takribani majuma mawili kupisha mashindano ya mapinduzi cup yanayoendelea huko visiwani Zanzibar.

Januari 13 kutakuwa na michezo mitatu ambapo Lipuli FC wao watakuwa nyumbani kuumana na mabingwa mara mbili wa Tanzania Bara Mtibwa Sugar mchezo ambao utafanyika katika uwanja wa CCM Samora mjini Iringa.

Chama la wana Stand United ya Shinyanga watakuwa katika uwanja wao wa nyumbani wa CCM Kambarage, kutafuta alama tatu muhimu zitakazowaondoa mkiani dhidi ya Ruvu Shooting ya Mkoani Pwani.

Siku hiyo itahitimishwa kwa mchezo wa Wanakuchele Ndanda FC ambao watawakaribisha wabishi Mbao FC katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Dabi ya Mbeya.

Jumapili yaani Januari 14 kutakuwa na mchezo mmoja pekee, mchezo wa Dabi ya jiji la Mbeya ambao utawakutanisha wajelajela Tanzania Prisons dhidi ya wanakomakumwanya Mbeya City.

Ligi hiyo itaendelea tena Januari 15 mwaka huu, Njombe Mji watacheza na wanankurukumbi Kagera Sugar katika uwanja wa Sabasaba mjini Njombe mchezo huo ukiwa ni nambari 100.

Yanga vs Mwadui

Mabingwa watetezi Dar Young Africans wenyewe watakuwa dimbani Januari 17 kucheza na wachimba Almasi wa maganzo mkoani Shinyanga Mwadui FC mchezo ambao utafanyika katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Wanalambalamba Azam FC watasafiri hadi mkoani Ruvuma kucheza na wanalizombe Maji Maji FC katika mchezo mwingine muhimu ambao utafanyika katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Raundi ya 13 itahitimishwa kwa mchezo mkali ambapo wekundu wa msimbazi na mabingwa mara 18 Simba SC watacheza na Singida United katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Vinara

Mpaka sasa Simba ndiye anayeongoza katika msimamo wa ligi hiyo akiwa na alama 26 sawa na Azam FC wanaoshika nafasi ya pili huku Singida United wakiwa nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 23.

Waburuza mkia katika ligi hiyo ni Ruvu Shooting wenye alama 11 wakiwa nafasi ya 14, Njombe Mji wenye alama 8 katika nafasi ya 15 na Stand United ambao wana alama 7 wakiwa katika nafasi ya 16.