VPL: Mtibwa waidondosha Yanga, Shooting akigawa pointi

Ligi kuu soka Tanzania Bara raundi ya 13 imeanza kwa kasi Jumamosi hii kwa viwanja vitatu kuwakaribisha miamba ya soka ambayo ilikuwa ikiwania pointi tatu muhimu kijisogeza kileleni mwa msimamo.

Mabingwa mara mbili wa Tanzania bara, Mtibwa Sugar wamesogea kileleni baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya wanapaluhengo Lipuli FC katika mchezo ambao umefanyika kwenye uwanja wa Samora mjini Iringa.

Mtibwa wakicheza kandanda safi walijipatia bao lao katika dakika ya 37 kupitia kwa winga wa pembeni Hassan Dilunga na kuzima ndoto za Lipuli kuwa na rekodi nzuri nyumbani kwao kwani huo unakuwa mchezo wa pili mfululizo kupoteza.

Ushindi huo unawafanya Mtibwa Sugar kujivuta hadi katika nafasi ya tatu wakiwa na alama 24 wakati Lipuli wao wakiendelea kuikamatia nafasi ya nane wakiwa na alama 15.

Ndanda 1-1 Mbao

Mkoani Mtwara katika uwanja wa Nangwanda Sijaona wenyeji Ndanda FC wamelazimishwa sare ya bao 1-1 na wageni Mbao FC mchezo ambao umetajwa kuwa mkali na wakuvutia katika dakika zote 90 za mtanange huo.

Wageni Mbao ndio walikuwa wakwanza kupata bao mapema kabisa katika kipindi cha kwanza kupitia kwa Emmanuel Mvuyekure na baadae wenyeji Ndanda wakasawazisha kupitia kwa Nassoro Kapama.

Matokeo hayo yanawafanya Ndanda kuchumpa hadi nafasi ya 10 wakiwa na alama 12 huku Mbao wao wakisalia katika nafasi ya 7 wakiwa na alama 15 kibindoni.

Stand United 1-0 Shooting

Mchezo mwingine siku ya Jumamosi umeshuhudia Ruvu Shooting wakiendelea kugawa pointi kama njugu baada ya kukubali kichapo kingine kutoka kwa Chama la wana Stand United cha bao 1-0.

Bao pekee la Stand United katika mchezo huo ambao umefanyika katika uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga limefungwa na Mrundi Blais Bigirimana na kuwafanya Stand United kujibandua mkia baada ya kukusanya alama 10, huku Ruvu Shooting wao wakiendelea kuikamata nafasi ya 14 kwa alama 11.

Dabi ya Mbeya.

Raundi ya 13 itaendelea tena Jumapili yaani Januari 14 ambapo kutakuwa na mchezo mmoja pekee, mchezo wa Dabi ya jiji la Mbeya ambao utawakutanisha wajelajela Tanzania Prisons dhidi ya wanakomakumwanya Mbeya City.

Ligi hiyo itaendelea tena Januari 15 mwaka huu, Njombe Mji watacheza na wanankurukumbi Kagera Sugar katika uwanja wa Sabasaba mjini Njombe mchezo huo ukiwa ni nambari 100.

Yanga vs Mwadui

Mabingwa watetezi Dar Young Africans wenyewe watakuwa dimbani Januari 17 kucheza na wachimba Almasi wa maganzo mkoani Shinyanga Mwadui FC mchezo ambao utafanyika katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Wanalambalamba Azam FC watasafiri hadi mkoani Ruvuma kucheza na wanalizombe Maji Maji FC katika mchezo mwingine muhimu ambao utafanyika katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Raundi ya 13 itahitimishwa kwa mchezo mkali ambapo wekundu wa msimbazi na mabingwa mara 18 Simba SC watacheza na Singida United katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Vinara

Mpaka sasa Simba ndiye anayeongoza katika msimamo wa ligi hiyo akiwa na alama 26 sawa na Azam FC wanaoshika nafasi ya pili huku Singida United wakidondoka hadi nafasi ya nne kwa kuwa na alama 23.

Waburuza mkia katika ligi hiyo ni Ruvu Shooting wenye alama 11 wakiwa nafasi ya 14, Njombe Mji wenye alama 8 katika nafasi ya 16 na Stand United sasa wana alama 10 wakiwa katika nafasi ya 15.

Related news
related/article
Local News
Njombe Mji: Yajayo dhidi ya Simba yawafurahisha
02 Apr, 16:49
Local News
AWCON 2018: She-Polopolo watua na mziki mnene kuwakabili Twiga Stars
02 Apr, 08:23
Local News
Azam Fc wakubali matokeo wahamishia nguvu kwenye ligi kuu
01 Apr, 19:45
Local News
ASFC: Singida United waangusha mbuyu, watinga nusu fainali
01 Apr, 18:10
Local News
ASFC: Stand United wajitapa kunyakuwa ubingwa
01 Apr, 12:03